Monday, January 15, 2007

SALAMU ZA MWAKA MPYA: UMUHIMU WA MATUMIZI BORA YA VIUATILIFU

Kutokana na changamoto nyingi nilizopokea tangu nianze kuandika katika ukurasa huu, nimeamua kutoa samu zangu za mwaka mpya wa 2007 kwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili. Mwanablogu Jeff Msangi aliwahi kuandika katika blogu yake kuwa kiingereza siyo lugha yake mama; wala siyo lugha ya pili, pengine ni ya tatu au ya nne. Hii ni hali halisi ya Watanzania walio wengi - waliozaliwa, kukulia na kusomea Tanzania. Hii pia inatokana na juhudi kubwa zilizofanyika huko nyuma kuikuza lugha hii. Pamoja na
ukweli kuwa lugha ya Kiingereza siyo lugha yetu mama bado ni muhimu kwa mawasiliano katika nyanja
ya kimataifa. Siyo nia ya makala haya kulinganisha lugha. Muhimu kwangu ni kuwa sijawahi kujuta kwa kuwa Mswahili na nimekuwa naheshimu sana mfumo wa elimu niliobahatika kupitia.

Katika salamu zangu hizi ninapenda kuongelea viuatilifu ambavyo kimsingi ni madawa ya kuua visumbufu vya mazao mashambani na hata katika maghala. Ni ukweli kuwa wengi tumekuwa aidha tunapuuzia kutumia madawa haya kwa uangalifu na kitaalamu na au hatujui jinsi ya kufanya hivyo. Sio nia yangu kutoa somo la namna ya kutumia na kutunza viuatilifu bali ni kutoa tahadhari juu ya madhara tunayoweza kupata. Nilipokuwa ningali kijana mdogo na nikiwa mtoto wa mkulima, nilihusika sana katika kupulizia madawa katika kahawa. Dawa maarufu sana katika shughuli hii ilikuwa Kopa ya bluu au nyekundu. Dawa hii ilichanganywa na DDT (kimatira) na nilikuwa napulizia shamba kubwa la babu yangu bila kinga (protective gears) zozote. Ni ukweli usiopingika kuwa wengi wetu hadi leo tumeendelea na mtazamo huu wa kutojali madhara ya madawa.

Asilimia kubwa ya Watanzania tunaishi vijijini ambapo chanzo kikubwa cha maji ni visima, mara nyingi visima vifupi. Ieleweke maji ya visima sehemu kubwa yanatokana na mvua kunyesha, kupenya na hatimaye kutuama katika kina fulani ndani ya ardhi. Hivyo madawa yasipotumika kitaalamu yaweza kuchafua maji haya na kusababisha magonjwa kama vile kansa. takwimu za hivi karibuni toka Taasisi ya Kansa Ocean Road zinaonyesha kuwa kila mwaka kuna idadi ya watanzania 20,000 wanaokutwa na tazizo la kansa. Inawezekana sehemu kubwa ya hawa hawatokani na matumizi holela ya viuatilifu. Hata hivyo kinga ni bora kuliko tiba.

No comments: